Jumapili 8 Februari 2026 - 21:00
Sheikh Ibrahim Zakzaky: Dunia inashuhudia mapambano kati ya uongofu na upotofu

Hawza/ Harakati ya Kiislamu ya Nigeria chini ya uongozi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky iliandaa hafla kubwa kutokana na mnasaba wa Nusu ya Shaaban na kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Mahdi (a.f.), iliyohudhuriwa na makundi mbalimbali ya wananchi katika mji wa Abuja.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ibrahim Zakzaky katika hafla hiyo alimpongeza Mwokozi wa wanadamu, Imam Mahdi (a.f.), na kumtambulisha kuwa mtetezi wa wanyonge duniani, huku akisisitiza kwamba hadi sasa yeye ndiye mwenye jukumu la kuongoza na kusimamia mambo katika Umma wa Kiislamu.

Akizungumzia maana halisi ya kungojea (Intidhar) alisema: Sisi hatungojei tu kudhihiri Imam Mahdi (a.f.) ili baada ya hapo tumfuate; bali hata sasa sisi ni wafuasi wake. Yeye ni kiongozi wetu na ndiye anayesimamia mambo yetu.

Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alieleza kuwa; dunia ya leo inaelekea wazi katika njia mbili zinazokinzana, akasema: Dunia daima imekuwa katika njia mbili za haki na batili, lakini leo njia hizi zimeonekana wazi zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Sheikh Zakzaky aliuliza: “Wakati zitakapo jitenga safu za haki na batili, wanafiki wataelekea upande gani?” kisha akasema: Bila shaka wataelekea upande wa batili.

Akirejea kuwa mapambano kati ya nguvu za uongofu na upotofu ni jambo lisiloepukika, alisema: Mapambano haya yatatokea bila shaka na hakuna njia ya kuyakwepa. Aliongeza kuwa maadui wa leo wanajionesha kuwa na nguvu, lakini kwa idhini ya Mwenyezi Mungu wameeleweshwa kuwa kuna nguvu iliyo juu yao, na kama hawatashambulia leo, watafanya hivyo baadaye, na huo ndio mwisho wao.

Kiongozi huyo pia alieleza kuwa; maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia yanayofanyika kwa jina la Mungu na katika njia ya Kiungu — hasa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran — ni miongoni mwa athari za uongofu na mafundisho ya Imam wa Zama (a.f.).

Akiweka mkazo juu ya kanuni ya Imama na uongozi wa Kiungu, alisema: Haiwezekani Mwenyezi Mungu kuiacha dunia bila hoja (Hujja).

Sheikh Zakzaky alisisitiza tena kwamba Imam Mahdi (a.f.) ndiye Imam wa kweli wa Umma wa Kiislamu, na akaonesha matumaini kwamba kudhihiri kwake kutatokea hivi karibuni.

Aliendelea kusema kuwa; dunia ya leo ni uwanja wa mapambano ya wazi kati ya nguvu za uongofu na upotofu, akiongeza kuwa watawala madhalimu wanawashambulia waumini na kuwatishia, lakini vitisho hivyo ni batili na visivyo na athari, na ahadi ya Mwenyezi Mungu haitoki nyuma.

Mwisho wa hafla hiyo, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria aliomba kuharakishwa kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.f.), na akamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie waumini wawe miongoni mwa wasaidizi na wafuasi wa kweli wa Imam huyo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha